Simulizi: Sioni kitu kingine namuona mama tu
Anna alikua na wasiwasi sana, kila wakati alikua akiangalia huku na kule kama atamuona Mama yake lakini hakumuona. Ilikua ni siku yake ya muhimu na alitaka Mama yake awepo pale, mara kadhaa alimuuliza Matrooni wake, akimuita MC kumuuliza Kama Mama yake amepatikana lakini wapi? Hakuna aliyejua Mama yake alikua wapi.
Alijikuta analia tu muda wote, hata muda wa kumtafuta mchumba wake na kumtambulisha mbele ya kadamnasi ulivyofika hakuwa na furaha. Alikua akilia na mumewe mtarajiwa alimtuliza, aliumia sana lakini alilazimika kuendelea, alijua kwa hali ya Mama yake labda alikataa kuja au alishatoroka tayari. Baada ya Send Off kuisha aliendelea kumtafuta hakumpata mpaka kesho yake.
Mama yake alirudi na alipomuuliza alikua wapi alikua akimuambia tu “Shetani! Shetani!” Akiwa amezaliwa na Mama ambaye hana akili nzuri (kichaa), Anna hakumjua Baba yake, Mama yake alipewa ujauzito na wapita njia wakati akiokota chakula jalalani, ndugu zake ambao walikua na uwezo mkubwa tu wa kifedha walishamtenga na hawakutaka kujihusisha nayeye kabisa, hivyo Mama yake alimlea mwenyewe mpaka alipochukuliwa na wasamaria wema.
Siku ya Harusi yake alijitahidi sana kuwa na Mama yake karibu, ingawa alikataa katakata kuvaa gauni zuri alilomnunulia lakini alitaka awepo na nguo zake zilezile chafu alizokua akishinda nazo jalalani. Kwake alikua akimuona kawaida hivyo hata wakati akipambwa alikua nje, hakutaka aondoke machoni kwake, safari ya kanisani alienda naye.
Hata watu walipojaribu kumzuia aliwaambia kuwa kama wakimzuia basi yeye anaondoka hawezi kufunga ndoa bila Mama yake, mchungaji alitumia busara akaruhusiwa, waliingia na kufunga ndoa. Njiani wakati wanaelekea ukumbini mume wake alikua amekasirika sana, ni muda mrefu alikua hataki kabisa Anna ajihusishe na Mama yake kutokana na hali yake lakini Anna alimuambia hawezi kumuacha Mama yake.
“Kwani ilikua ni lazima umlete Kanisani, haya kashakuja kaharibu picha na ukumbini nako unataka aingie!” Mumewe aliongea kwa hasira. Anna bila kutetereka alimuambia Mama yangu ndiyo kila kitu siwezi kumuacha mwenyewe, hana mtu mwingine wa kumhudumia atakua peke yake. “Mimi simtaki kwenye harusi yangu, utafute sehemu ya kumpeleka, kama usipotafuta nitamtafutia mimi kama nilivyofanya kwenye Send Off!”
Mumewe aliongea kwa hasira, Anna alimuuliza alimfanya nini kwenye Send Off lakini mumewe hakujibu, alimuambia yeye hawezi kuharibu harusi yake kwa kualika vichaa, akiuliza ndugu zake watamuelewaje? Anna hakujali, aliapa nilazima Mama yake aingie, walifika ukumbini lakini kabla ya kuingia Mama yake alichukuliwa na ndugu wa mume wake, na alipouliza aliambiwa anaenda kuoneshwa sehemu ya kukaa.
Aliingia ndani lakini hakumuona Mama yake, siti ya Mama yake ilikua wazi. Aliendelea kumuangalia mpaka ulipofika wakati wa kutambulisha ndugu hakumuona, ilikua ni zamu yake kutambulisha ndugu zake na ndugu pekee wa upande wake alikua ni Mama yake, wengine walikua ni marafiki na majirani, ndugu wa damu wa Mama yake hawakutaka kuhudhuria kabisa ingawa aliwaalika.
Alipewa kipaza sauti kuongea, kama dakika tano alisita alishindwa kuongea. Mumewe aliona na kutaka kuchukua kipaza sauti ili amsaidie kutambulisha lakini alikataa, alisema “Nitaongea mwenyewe.” Alitulia kidogo kisha akaendelea. “Nimepewa kipaza sauti ili nitambulishe ndugu zangu, lakini nikiangalia hapa hakuna ndugu yangu hata mmoja,sanasana namuona Mama mwenye nyumba wangu, majirani na marafiki, lakini hakuna ndugu…”
Alitulia kidogo, mumewe alimuangalia kwa hasira. Alimuonyesha ishara aongee harakaharaka lakini yeye aliongea taratibu akihakikisha kila mtu anasikia “Mimi nimezaliwa peke yangu kwa Mama, kwa Baba sijui kwani simfahamu Baba yangu. Mama yangu ni yule ambaye wengi wenu mkimuona mtasema ni kichaa, mtasema hana akili nzuri lakini mimi nikimuangalia namuona kama Mama, sioni kitu kingine.
Namuona kama Mama ambaye miaka 27 iliyopita wakati akiwa jalalani mchafu anakula vyakula vilivyotupwa na wengine, alikua akishindana na Mbwa kuokota chakula! Lakini kwa hali hiyo hiyo akiwa ametengwa na ndugu zake kuna mwanaume alimfuata na kumpa mimba, na pale pale jalalani bila msaada wa mtu yeyote nilizaliwa, alininyonyesha, akanivalisha na sikukosa chochote.
Huyo ndiyo mwanamke ninayemuona leo, alinilinda na kila aina ya adui na kila nilipolia alinibembeleza kama mnavyobembeleza watoto wenu.” Alitulia na kufuta machozi, watu bado walikua wakishangaa. “Nilipofika umri wa kwenda shule, yeye mwenyewe, pamoja na watu wote kumuona kichaa alinibeba na kunipeleka shuleni, hakujua naenda kufanya nini lakini aliona watoto wenzangu wanapelekwa huko akanipeleka.
Nilipokelewa na nilianza shule na hata watu walipotaka kunichukua alinilinda na niliendelea kukaa palepale jalalani mpaka alipotokea msamaria mwema na kunisomesha. Alinichukua kutoka kwake lakini hawakuuchukua moyo wangu kwake, ingawa mtu aliyenichukua mtaani hayupo leo hapa kwani katangulia mbele ya haki, lakini bado Mama yangu aliendelea kubaki mzazi pakee.
Nilipomaliza Chuo nilijaribu kumbadilisha, kumnunulia nguo nzuri lakini alikataa na alishindwa kuwa kama nilivyokua ninataka mimi ndipo nilipogundua kuwa sikupaswa kumbadilisha ili nimfurahie, bali kumpenda kama alivyo kwani mimi alinipenda kama nilivyo. Sasa watu wote mnamuona kichaa lakini mimi namuona kama Mama na sitaki abadilike nampenda hivyo hivyo alivyo.
Katika Send Off yangu nililia sana kwani hakuwepo na nilijua labda katoroka na kurudi jalalani, lakini leo nimegundua kuwa kumbe mume wangu mpendwa ndiyo alimtorosha na kumpeleka mbali ili tu nisiharibu picha za Send Off, lakini leo sasa hivi pia simuoni na nimekuja naye hapa ukumbini naamini mume wangu niwewe pia umemchukua ili asionekane na watu ukapata aibu.”
Alitulia kidogo, MC alitaka kumnyang’anya kipaza sauti lakini alikataa, huku akijikaza machozi ya simtoke alisema. Nakupenda sana mume wangu na leo tumekua mwili mmoja, lakini kama hutaweza kumheshimu mwanamke aliyenileta duniani eti kwakua yeye havai kama unavyovaa wewe, hali chakula kama unachokula wewe na hana akili kama ulizonazo wewe basi siwezi kuishi na wewe kama mume wangu.
Samahani lakini hapana, nimeamua kumchagua Mama yangu kuliko wewe kama alivyonichagua mimi, kwaheri narudi jalalani kumfuata mama yangu.” Alimaliza kuongea huku akivua pete ya uchumba na ya ndoa, alitupa chini na kukimbia kutoka nje. Mumewe alimkimbilia, alimfikia na kumpigia magoti ili kuomba msamaha. Aliongea maneno mengi lakini hakumsamehe alimuambia anamtaka Mama yake kwanza.
Sherehe ilisimama kwa masaa mawili. Mama yake alipatikana na aliruhusiwa kuingia ukumbini. Bwana harusi alipiga magoti mbele za watu na kumuomba msamaha Mama mkwe wake pamoja na Anna mkw wake, alionekana kujutia na Anna alimsamehe. Walisherehekea na hata wakati wa chakula, kwa heshima ya Mama yake Anna ambaye alikua hawezi kula chakula kilichopo kwenye sahani akiita sumu, wageni wote walikula chakula katika vimfuko vyeusi.
Hakukua na kijiko, Bufee iliweka chakula katika vimfuko vyeusi ambavyo vilinunuliwa usiku uleule na kila mtu alikula. Mama yake alifurahi sana kuona kila mtu anakula kama yeye. Anna kila saa alimuangalia Mama yake na kutokwa na machozi, watu walimpongeza kwa upendo aliouonesha na namna alivyokua akijivunia kuwa na Mama kama yule. Hakumuona kama kichaa au mtu aliyachanganyikiwa, mchafu alimuona kama Mama”.
Je umejifunza nini kupitia hii simulizi? andika hapo chini maoni yako juu ya kile ulichojifunza.
0 comments:
Post a Comment