Panapo majira ya usiku kabla sijalala nikakumbuka na kutafakari juu ya huu mfano ambapo inawezekana na wewe umeshawahi kuusikia sehemu.

Kulikuwa na muwindaji mmoja msituni, siku moja katika pitapita yake akaliokota yai la Tai ( Eagle ) , akaamua alichukue akaenda nalo kwake akalichanganya na mayai ya kuku wake. Kuku akaatamia yale mayai hatimaye siku moja akayaangua likiwemo na yai la tai. Yule tai akakua pamoja na wale vifaranga wa kuku akiamini kuwa yeye ni kuku, na akiwa na tabia zote za kuku. Lakini siku moja wakati wapo porini aliangalia juu akamuona tai mwenzake anaruka juu zaidi, akauliza wenzake ambao ni kuku yule anayeruka jui ni nani? Mbona anafanana na mimi! Wenzake wakamjibu ndiyo anafanana na wewe ila mwenzako anauwezo mkubwa sana,  kwanza ni ndege ambaye anaruka juu sana kuliko sisi. Na pia wewe huwezi kuwa kama yeye kwa sababu upo kama sisi na tumekuwa wote pamoja. Kwa hiyo muache tu yule aendelee kututawala. Yule tai aliyepo chini alikufa akiamini kuwa na yeye ni kuku.

Tafakari
Sisi tumeumba kuwa watawala kama tai, ila tunaishi miongoni mwa kundi la watawaliwa ( kundi la kuku ). Na mara nyingi sana wamekuwa wakitukatisha tamaa kwa maneno mengi sana kama: wewe huwezi kuwa kama yule, mwenzako ametoka kwenye familia ya matajiri ndo maana kawa tajiri au mwenzako ana bahati siyo kama wewe au wewe huwezi kuwa tajiri kwa sababu hata elimu huna. Na kundi hili lenye kusema haya maneno mara nyingi wao huwa maisha yao yote wanaamini kuwa hawawezi kufanya vitu vya kwao kama wanavyofanya waliofanikiwa kama wakina Mengi, Bakhresa, Billigate na wengineo matajiri.

Tunajifunza nini kutoka katika stori hii.
  1. Wewe umeumbwa na uwezo mkubwa sana ( uwezo wa tai ) ila ni kwamba haujajitambua kuwa wewe ni nani na kuishi maisha kama ya kuku.
  2. Dunia ina wakatishaji tamaa wengi sana, ukiwasikiliza hautaweza kuishi maisha unayoyatamani ambayo Mungu amekupangia.
  3. Kuzaliwa na kukua miongoni mwa kundi la watawaliwa isikufanye ukashindwa kuishi maisha ya mtawala.

Usikubali kufa kama kifo cha tai aliyeamini kuwa yeye ni kuku na akashindwa kuutumia uwezo wake mkubwa aliokuwa nao.

Nakutakia tafakari njema.

0 comments:

Post a Comment

 
Top