Kwa nini usifaulu darasani?
Miaka ya nyuma nilipokuwa mdogo nakumbuka wazazi wangu walikuwa wananisisitiza sana kwenye masomo, ilikuwa siwezi kwenda kucheza bila kusoma kwanza. Nikishamaliza kusoma ndo walikuwa wananiruhusu kwenda kucheza na wenzangu. Na hiyo ilinisidia sana hata katika mitihani yangu kufanya vizuri tofauti na wenzangu ambao kila muda walikuwa wanacheza pasipo kusoma. Ni kwa nini basi walikuwa wananifanyia hivyo! ni kwa sababu walikuwa na malengo ya mimi kufika mbali
Leo ningependa kuongea na rafiki zangu wanafunzi popote walipo iwe ni Tanzania au ni nje ya Tanzania hususani kwenye vitu ambavyo ukiwa kama mwanafunzi unatakiwa uvizingatie kwenye usomaji wako ili uweze kufaulu katika masomo yako. Kwa kusoma hii makala utaweza kufahamu ni kwa nini wanafunzi wanafeli darasani. Tuanze kuviona hivyo vitu muhimu vya kuvizingatia katika usomaji:
🚤Bidii na Juhudi katika usomaji.
Kama tunavyojua katika kila kitu unatakiwa ukifanye kwa juhudi na bidii zote. Kama ilivyokuwa kwangu mzazi wangu alikuwa anahakikisha nakuwa na juhudi na bidii ya kusoma ndipo alipokuwa ananiruhusu kwenda kucheza. Kama ni mwanafunzi hakikisha kwamba unasoma ndipo ufanye kitu kingine. Kama ni weekend hakikisha kwanza unasoma ndipo unaenda kufurahia weekend. Na unaposoma soma kwa bidii ukimaanisha na hii itakuweka katika nafasi nzuri ya kufaulu.
Bidii na juhudi pia inahusisha kuhudhulia darasani wakati wa vipindi, usiwe doja maana itakufanya utumie nguvu nyingi sana katika usomaji. Unapohudhulia vipindi darasani itakupa urahisi wa kusoma na kuelewa zaidi pindi utakapokuja baadaye kujisomea.
🚤Kuwa na ratiba ya usomaji.
Ni kitu muhimu sana kwa mwanafunzi kuwa na ratiba ya kujisomea ( Timetable ) , na hiki ndo kitu kinachowashinda wanafunzi wengi. Wengi wanasoma pasipo ratiba wanasoma kwa kukurupuka, akijisikia kusoma hesabu anaenda kusoma hesabu, akijisikia kusoma Uchumi anabeba daftari la uchumi. Huu siyo usomaji kwa sababu kuna masomo utakuwa hauyatendei haki na hautaweza kuyafaulu. Panga ratiba yako ya kujisomea itakayokuongoza katika usomaji na kwa kufanya hivi utakuwa na nafasi nzuri ya kufaulu katika masomo yako.
🚤Kuwa na malengo katika usomaji wako.
Haitoshi tu kuwa na ratiba ya usomaji bali pia unatakiwa uwe na malengo katika usomaji wako. Usisome ili mradi umesoma, usomaji haupo hivyo. Kama kweli unataka kufaulu katika masomo yako soma ukiwa na malengo. Kupata A katika mtihani huwaga siyo muujiza kama unabisha waulize wanaopata A darasani, watakuambia kuwa walikuwa na malengo ya kupata A na ndiyo maana wamepata. Kuna watu usomaji wao ni wa kaiwaida tena usio na malengo, haujawahi kuwasikia watu (wanafunzi) wakisema mimi hata nikipata C inanitosha ili mradi tu nisifeli, kwa uchunguzi wangu niliofanya watu wengi kama hawa ndo wanaoongoza kwa kufeli darasani. Ila siyo wote wengine huwa na sababu zingine.
Acha kusoma bila kuwa na malengo, panga alama ( maksi ) ambazo unataka kupata katika mitihani yako hii itakusaidia hata pale utakapokuwa unasoma itakupa motisha katika usomaji wako. Panga unataka kupata A ngapi au B ngapi na hii itakusaidia.
🚤Kusoma vitabu.
Yah! kama unataka kuja kuwa mwanafunzi anayefaulu darasani hakikisha unakuwa na tabia ya kusoma vitabu. Usiishie tu kusoma kile kitu ambacho umefundishwa darasani. Kumbuka mwalimu anakufundisha kwa asilimia 25 tu, hizi asilimia zilizobakia 75 unatakiwa ukazitafute mwenyewe, na utazipata pale unaposoma vitabu pamoja na matilio mengine.
Ni vizuri pia kusoma hata vitabu vilivyotofauti na darasani vinaweza vikawa ni novo au vitabu vya uhamasishaji au biashara, na kwa kufanya hivi itakusaidia kuwa na uelewa mpana hata katika masomo yako darasani.
🚤Kutosoma msuli wa zima moto.
Kwa wanafunzi wananielewa, nilipokuwa shuleni kuna jamaa zangu wao usomaji wao walikuwa wanangojea siku za mitihani ndipo wasome sana, na wanakesha madarasani usiku kucha wakisoma. Hii haitakusaidia kama kweli unataka kufaulu kwa alama za juu darasani. Kwanza unakuwa unaupa kazi ubongo wako na kuuchosha kwa kuangaika kushika vitu vingi kwa wakati mmoja, matokeo yake unapoingia kwenye mtihani unasahau vitu vingi. Ndo maana kuna watu wakitoka kwenye mtihani ndo wanakumbuka majibu ya maswali wakati wameshatoka kwenye chumba cha mtihani, na hii yote ni kwa sababu ya msuli wa zima moto. Ewe mwanafunzi unatakiwa kusoma kila siku, panga ratiba yako vizuri usisubili kipindi cha mtihani kifike ndipo uanze kusoma, hautafanikiwa na kama ukifanikiwa ni kwa kufaulu maksi za chini usizozipenda.
Ni matumaini yangu umejifunza kitu na kinachotakiwa baada ya kusoma makala hii ni wewe kuwa na mikakati katika masomo yako. Na hakika utaona mafanikio.
0 comments:
Post a Comment