Kulikuwa
na familia moja maskini sana. Ilikuwa familia ndogo ya baba, mama na binti yao
wa pekee. Baba ndiye alikuwa mtu pekee mwenye kipato, hata hivyo kipato chake
kilikuwa kidogo sanaa kilichoweza kuwasaidia kujikimu mahitaji muhimu tu japo
pia hakikutosha. Baba alimpenda sana binti yake na alijitahidi sana kufanya
kazi za vibarua ili apate pesa za kumsomesha mwanaye aliyekuwa na ndoto za kuwa
daktari. Alimpenda sana binti yake, binti ambaye alikuwa na uwezo mzuri
darasani, alifaulu mitihani yake kwa maksi za juu sana, kila mtu alimpenda kwa
uwezo wake.
Ilikuwa
ni siku ya matokeo yake ya shule ya sekondari kidato cha sita. Kwa mara
nyingine alikuwa amefaulu vizuri kama kawaida yake, Baba yake alifurahi mno
akamtaka mwanae aombe chochote kile anachokitaka kama zawadi atamnunulia. Binti
akamwambia, " baba nataka gauni
ambayo nilikuonyesha siku ile tulipokwenda kutembea, siku ile nilishindwa
kukwambia kwakuwa gharama yake ni kubwa mno, elfu 50. Lakini kwakuwa leo
umeniruhusu kuomba chochote kama zawadi nimechagua gauni." Baba yake
hakujali ukubwa wa gharama, alichotaka ni kumuona binti yake wa pekee akiwa na
furaha. Hivyo akaahidi kumnunulia. Kesho yake akaenda mjini akarudi na gauni la
binti yake. Mke wake alijua fika mume wake hakuwa na fedha za kumudu kununua
gauni hilo, hivyo akamuuliza wapi amepata kiasi hicho kikubwa cha pesa. Baba akajibu,
"Nilikuwa na akiba kidogo lakini pia nikaamua kwenda hospitali kuuza damu
yangu ili nipate fedha za kuongezea kununua gauni, sikutaka kumfedhehesha binti
yangu"
Muda
ukapita, binti akaanza chuo kikuu cha udaktari. Baba yake aliuza karibu kila
kitu ili kulipia gharama za chuo. Aliuza vitu vyote vya ndani hadi kitanda
wakabaki wanalala chini yeye na mke wake. Aliyafanya yote hayo kwakuwa alimpenda sana binti yake
na alitamani kuona ndoto za mwanae za kuwa daktari zinatimia. Binti akasoma,
hatimaye mwaka wake wa mwisho wa masomo ukafika. Wakati anakaribia kuanza
mitihani ikaonekana kuwa hajamaliza kulipa ada, hivyo hatoweza kufanya
mitihani. Sasa baba hakuwa na kitu cha ziada cha kuuza, hatahivyo hakutaka
kumuangusha binti yake. Akaondoka akarudi kesho yake na kiasi cha fedha cha
kutosha, akampa binti yake akalipe ada. Lakini tena Mke wake akagundua wazi
kuwa mumewe hakuwa na fedha wala sehemu ya haraka ya kupata fedha nyingi kiasi
kile, hivyo akamuuliza wapi amezipata fedha zile. Baba akajibu, "Sijafanya
jambo baya, sikutaka kumuangusha mwanangu. Kuna tajiri alikuwa na matatizo ya
figo hospitalini, hivyo alitakiwa kupewa figo mpya maana figo yake ilikufa, nikaamua
kumuuzia figo yangu moja ili nipate pesa kwa ajili ya binti yangu, lakini
tafadhali usimwambie, atajihisi mwenye hatia akijua nilifanya hivi kwa ajili
yake. " Mke wake alisikitika kwa kuwa alijua figo aliyoitoa mume wake ni
nzima lakini hiyo moja iliyobaki ina matatizo kwa hiyo inaweza kufeli muda
wowote. Kweli, muda si mrefu baba alianza kuumwa. Baba alidhoofu, alikonda
sana. Alimuomba Mungu asife mpaka ashuhudie Siku ambayo mwanae anavalishwa taji
na kukabidhiwa cheti chake cha heshima cha Udaktari.
Siku
ikafika, ilikuwa ni siku ya Mahafali. Baba na mama walijiandaa kwa furaha
kumpokea binti yao. Waliandaa kasherehe kadogo ka familia kumpongeza binti yao.
Walimsubiria kwa hamu daktari mpya. Muda ukawadia, Binti akaja, ndiyo binti
alikuja lakini alikuja akiwa Maiti....Ndiyo alikuwa Maiti, amebebwa kwenye
jeneza!!....Usiku wa kuamkia siku ile ya mahafali alimfumania mpenzi wake,
hakuwa tayari kuuvumilia usaliti ule, akaamua kunywa sumu, akaamua kuukatisha
uhai wake!!. Ndoto zake zote zikazima ghafla. Hakuna aliyeamini tukio lile. Baba
aliumia sana kumuona binti yake mpendwa akiwa amekufa, akapata mshtuko wa moyo,
akafariki palepale. Misiba ikawa miwili kwa siku moja.
FUNDISHO:
Mara nyingi tunafanya maamuzi bila kujua ni kwa kiasi gani yatawaathiri wale
wanaotupenda kwa dhati, wale wanao tumia
muda wao mwingi kutupa furaha. Tunaharibu mwelekeo wetu wa maisha sababu ya
kufanya maamuzi yasiyo sahihi katika maisha. Tunawafurahisha wale wasiojua
thamani yetu na kuwaumiza wale wanaotuthamini kwa kila hali. Mungu akupe
kufanya maamuzi sahihi, maamuzi ya kukupa wewe furaha na sio kuwapa wengine
furaha wakati hawaithamini hiyo furaha.
0 comments:
Post a Comment