Siku moja mwanamke alitoka nje ya nyumba na kuwaona wazee watatu wenye mvi kichwani wakiwa wamekaa nje ya nyumba yake.

Hakuwatambua na wala hakuwa anawafahamu.

Akawaambia, "nafikiri siwafahamu, ila inavoonesha mna njaa sana. Tafadhali wazee wangu mkaribie nyumbani kwangu japo mpate hata chakula"

"Baba mwenye nyumba yupo?", mmoja wa wale wazee aliuliza.

"Hapana" yule mwanamke alijibu "Ametoka kidogo."

"Basi hatuwezi kuingia ndani", wale wazee walimjibu.

Jioni mume wake aliporudi, mke alimueleza kilichotokea.

"ah wale wazee watatu nami nimewaona hapo nje ila sikutaka kuwatilia maanani, nenda kawaambie nimerudi na wakaribishe ndani" Mume alimwambia mkewe.

"Hatuwezi kuingia ndani ya nyumba yenu sisi sote", wazee walijibu baada ya mke kuwaambia kwamba mumewe amerudi na anawahitaji.

"Kwanini?" mke alitaka kujua.

Mmoja wa wale wazee akamuelezea: "Huyu mwenzangu (huku akimshika bega mzee mwenzake) anaitwa UTAJIRI, na huyu mwingine (huku akimnyoshea kidole) anaitwa MAFANIKIO na mimi ninaitwa UPENDO."
baada ya kujitambulisha yule mzee akamwambia yule mwanamke, "sasa nenda ndani ukajadiliane na mume wako nani kati yetu aingie ndani ya nyumba yenu, yaani Utajiri, Mafanikio au Upendo"

Mwanamke akaingia ndani na kumueleza mume wake yale aliyoambiwa na Mzee upendo. Mume wake alifurahi sana. Akasema, "vizuri sana, kwa kua ndio hivyo basi tumkaribishe UTAJIRI aingie ndani ya nyumba yetu, muache aje ndani ya familia yetu na atupe utajiri"

Mke hakukubaliana na matakwa ya mume wake. "Mpenzi kwanini tusimkaribishe Mzee MAFANIKIO?"

Wakiwa wanaendelea kubishana, binti yao mdogo aliyekuwa akiwasikia wakibishana akaja na mawazo yake, binti akasema: "Je haitakuwa vema tukimkaribisha Mzee UPENDO?, nyumba yetu itajazwa na upendo. Kwa maana humu kila siku imekuwa ugomvi tu, baba na mama mnagombana na kupigana mimi bila kujua sababu."

"Tumuache binti yetu aamue, nenda na ukamkaribishe Mzee UPENDO kama binti yetu alivyopendekeza" Mume aliongea.

Mke alitoka nje na kuwauliza wale wazee watatu, "Mlisema ni nani kati yenu anaitwa Mzee UPENDO? Tafadhali sana karibu nyumbani kwetu na uwe mgeni wetu."

Mzee UPENDO akanyanyuka na kuanza kufuatana na yule mwanamke. Wale wazee wawili waliobaki nao wakaanza kufuata nyuma.

Kwa mshangao yule mwanamke akauliza nimemualika Mzee Upendo tu, na ninyi ndivyo mlovyosema kwamba hamuwezi kuingia wote, sasa iwaje nanyi wawili mnakuja ndani?

Wazee wote watatu kwa pamoja wakajibu: "kama ungalikuwa umemualika kati ya UTAJIRI au MAFANIKIO, wawili tungalibaki nje, ila kwa kuwa umemualika UPENDO popote atakapoenda sisi tutamfuata.

Baada ya Upendo kuingia ndani ya nyumba, upendo ulitamalaki ktk familia, amani ya roho ikawepo, utajiri ukajisogeza zaidi na mafanikio wakayapata.


Popote penye upendo kuna utajiri na mafanikio. Upendo ni dhana pana sana Paulo anasema, "Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainisaidii kitu.

Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya;

Haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; Huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote."

Mwenyezi Mungu atuongoze ili Upendo, utajiri na mafanikio viwe na sisi daima.

0 comments:

Post a Comment

 
Top