Kengele ya kutoka darasani iligongwa, wanafunzi wa shule ya msingi wakaanza kutoka madarasani huku wakifukuzana wengine wakipiga kelele ilimradi shwangwe tu.
Ilikuwa mara yangu ya kwanza kufundisha shule za hatua hiyo.
Ilikuwa ni shule ya serikali.
Jicho langu liliangukia katika sura ya msichana mdogo, nguo zake chafu. Alikuwa analia.
Alikuwa peke yake na hakuwa na yeyote wa kumbembeleza.
Mimi kama mwalimu sikutaka kujisogeza karibu naye sana. Kwanza nilikuwa mgeni.
Nikaachana naye.
Siku iliyofuata tukio kama lile likajirudia. Msichana yuleyule wakati ule uleule wa kutawanyika, alikuwa analia sana. Mwishowe aliondoka huku akiwa analia.
“Mbona mwenzenu analia?” nilimuuliza mwanafunzi mmoja.
“Huyo ni mama kulialia..” alinijibu huku anacheka.
Haikuniingia akilini hata kidogo kuwa yule binti analia bila sababu.
Siku ya tatu nikaanza kujiweka karibu naye.
Muda wa mapumziko nilimwita nikamnunulia chai, alikuwa ananiogopa na hakutaka kuniangalia machoni.
Sikumuuliza lolote juu ya tabia yake ya kulia lia kila anaporuhusiwa kurejea nyumbani.
Hata siku hiyo pia alilia vilevile. Wenzake wakawa wanamzomea.
Akili yangu iligoma kuamini kuwa binti yule analia bila sababu.
Kwanini alie wakati wa kutawanyika tu?? Hapana si bure.
Nikaendelea kujiweka karibu naye. Mkuu wa shule akafikishiwa taarifa kuwa nina mahusiano ya kimapenzi na yule mtoto.
Moyo wangu na Mungu pekee ndio walikuwa mashahidi. Nilikosa cha kujibu.
Nilijaribu kujiweka mbali naye lakini moyo ulinambia kuwa kuna jambo natakiwa kulijua.
Nikaendelea kuwa karibu naye. Hatimaye mkuu wa shule akanisimamisha kufundisha pale kwa tabia yangu ya kufanya mapenzi na mwanafunzi.
Nilijitetea lakini sikueleweka. Nikamwachia Mungu……
Licha ya kusimamishwa kazi, niliendelea kufuatilia nyendo za yule binti aliyeitwa Janeth.
Kila alipotoka shule nilimvizia njiani na kumnunulia chakula, kisha tunazungumza kidogo.
Aliponiamini kama kaka yake ndipo nikajieleza dukuduku langu.
“Janeth…” nilimuita.
“Bee kaka ….” Aliitika huku akinitazama.
“Nyumbani unaishi na wazazi.”
“Ndio naishi na mama..baba huwa anasafiri safari.”
“Mama yako ana watoto wangapi?”
“Mama yangu alikufa….alikufa nikiwa mdogo hata simkumbuki” Alijibu kwa sauti ya chini.
“Kwa hiyo unaishi na mama mdogo.”
“Ndio.”
“Unampenda mama mdogo?”
Swali hili likaikatisha furaha ya Janeth. Akaanza kulia, alilia bila kukoma, Janeth alilia kwa uchungu hadi nikajisikia vibaya. Nilimbembeleza kisha sikumuuliza tena.
Siku zikaenda bila kumuuliza chochote..
Baada ya siku kumi, ilikuwa siku ya michezo pale shuleni, hivyo hapakuwa na masomo.
Janeth alichelewa kuja shule, nilimngoja uwanjani, hadi alipofika majira ya saa nne.
Nikamwambia twende kunywa chai.
Siku hiyo nilimpeleka mbali kidogo, tukanywa chai, kisha tukakaa mahali palipokuwa wazi.
Nikaleta tena mjadala mezani.
Ni kuhusu maisha ya Janeth.
Alikataa kabisa kusema lolote, nilimshawishi sana.
“Usiogope mimi ni kaka yako.” Nilimpooza.
Janeth badala ya kusimulia akaanza kulia tena.
“Ataniua mama nikisemaaaa” alilalamika.
Nikambembeleza hatimaye akanieleza jinsi anavyonyanyaswa na mama yake.
“Mama hanipendi hata kidogo, ananipiga na kuninyima chakula, hapendi nije shule, vyombo tunavyotumia usiku hataki nivioshe usiku na hataki niwahi kuamka asubuhi, nikiamka natakiwa kufanya kazi zote, kufagia uwanja, kudeki nyumba, kuosha vyombo kisha ndipo nije shule. Baba akiwepo anajidai kunijali sana…”
Alijieleza.
“Ni hayo tu Janeth….niambie kila kitu.”
“Akijua ananiua alisema….”
“Kwani amewahi kukutesa vipi..”
Ni hapa Janeth alivyozungumza huku analia kilio ambacho hakitatoka masikioni mwangu kamwe.
Siku moja, alichelewa kuamka, ilikuwa siku ya mapumziko.
Mama yake alipomwamsha, aliitika na kupitiwa usingizi tena.
Mama aliporejea mara ya pili, alikuwa na mti mkavu, alimpiga nao kichwani na popote pale katika mwili, alipoona hiyo haitoshi akamvua nguo, akausokomeza katika sehemu za siri, aliuigiza hovyohovyo, ukuni huo ulikuwa wa moto.
Yeyote mwenye moyo wa nyama ajifikirie ukuni wa moto ukazamishwa sehemu za siri za mtoto wa darasa la sita.
Nilitokwa machozi.
Nikawahi kujifuta hakuona.
“Baba yeye alisemaje….”
“Baba ni mkali na hapendi kunisikiliza na mama aliniambia nikiambia mtu ananiua mara moja.” Alijibu kwa huzuni.
“Nikija na dada yangu tunaweza kukuona ulivyounguzwa..”
“Ndio…” alinijibu.
Sikutaka kulaza damu nikampigia simu rafiki yangu wa kike.
Nikamuuliza kama yupo kwake, alikuwepo.
Nikaongozana na Janeth.
Tukafika, Janeth akatoa nguo zote.
Ilihitaji moyo wa kiuaji sana kutazama mwili wa Janeth mara mbilimbili.
Alitisha, hakika alikuwa ameunguzwa vibaya na vidonda vilikuwa havijapona vizuri.
Dada yule alishindwa kujizuia alimlazimisha Janeth twende kwa mama yake amkabiri na kumpa kipigo. Nikamzuia.
Hata mimi nilikuwa na hasira kali. Lakini sikutaka kuiruhusu ifanye kazi.
Nikachukua kamera, nikampiga picha Janeth katika yale makovu.
Mbio mbio nikaenda polisi, kituo cha haki za watoto nikaelezea mkasa ule huku nikishindwa kujizuia machozi.
Nikawaonyesha na picha.
Tukaongozana nao hadi nyumbani kwao Janeth.
Mama yule akakamatwa bila kutarajia.
Nilitamani kumrukia nimng’ate lakini haikuruhusiwa.
Sheria ikafuata mkondo. Janeth akaanza kupokea tiba.
Yule mama akahukumiwa kwenda jela miaka sita..hadi sasa yupo jela.
Mume wake alitozwa faini kubwa kwa kosa la kutofuatilia maendeleo ya mtoto wake kiafya……..
Mimi nilirudishwa kazini, kwa heshima kubwa. Heshima ya kumkomboa mtoto.
0 comments:
Post a Comment