Kijana mmoja alisafiri kwa meli na rafiki zake, wakiwa katikati ya safari yao meli ilianza kuzama. Watu wengi pamoja na rafiki wa yule kijana walikufa maji wakati wanajaribu kujiokoa kwa kuogelea, lakini yule kijana alifanikiwa kushika ubao ulioelea majini akaanza kuelea nao, maji yalimpeleka hadi kisiwa cha mbali sana ambako hakukuwa na watu wala wanyama isipokuwa wadudu tu! Alifika ufukweni amechoka sana na asiyeamini tukio lililotokea, akaishi huko kwa kula matunda. Aliweza kujenga ka-kibanda kwa shida sana maana hakuwa na shoka wala panga, hatimaye akaanza maisha mapya.
Aliishi muda mrefu kisiwani na tayari alishazoea mazingira yale ya shida japo shida haizoeleki. Mara zote nyakati za jioni aliwasha moto kwa kupekecha vijiti. Siku moja kama kawaida yake aliwasha moto nje karibu na kibanda chake, aliota moto muda mrefu hatimaye akapitiwa na usingizi. Alilala hapo hapo hadi usiku wa manane aliposhtushwa na joto kali lisilo la kawaida. Kumbe moto ulishika nyasi za kibanda chake na kibanda chote kikaungua moto.Alilia sana na kumlaani sana Mungu kwa mateso hayo akisema "Hivi Mungu nimekukosea nini mpaka unitese hivi? Pamoja na shida zote hizi bado unaniongezea shida nyingine, umeteketeza makazi yangu ilhali nimejenga kwa shida, Hukuridhika kunitenga mbali na familia yangu nilipoishi kwa raha? Hukuridhika kuwaua rafiki zangu wote baharini? Kwanini Mungu umekuwa mkatili hivi? Bora nife tuu maana nimeshachoshwa na hizi shida!" akaendelea kulalamika na kumlaani Mungu hadi kukapambazuka.
Ilipofika asubuhi aliiona meli ikija kwa mbali kuelekea alipo, alishangaa maana hakuna meli yoyote inayoweza kwenda kisiwa kile labda kama imepotea njia. Meli ilipofika ufukweni yule kijana akaifuata, alienda moja kwa moja hadi kwa kapteni.Kapteni akamwambia "tuliona moto mkali sana usiku tukahisi ni meli inawaka moto tukasema tuje ili tutoe msaada..kwa kweli tumetembea masaa mengi sana hadi kufika hapa, mshukuru Mungu maana ametumia moto kutuleta hapa" yule kijana kusikia hivyo alilia sana, akajilaumu kwa jinsi alivyo mnung'unikia Mungu. Akaelewa kuwa Mungu ana njia nyingi za kuleta msaada kwa mtu. Akapiga magoti akatubu huku akimshukuru Mungu. Safari ya kurudi nyumbani ikaanza.
FUNDISHO: Wakati mwingine Kuna mambo mabaya huwa yanatokea katika maisha yetu yanayotufanya tuone kama Mungu ametusahau. Tunamnung'unikia na kumlaumu Mungu bila kujua kuwa Mungu ana njia nyingi sana kutuletea msaada. Njia za Mungu huwa zinaonekana kama ujinga fulani, lakini kiukweli ujinga wa Mungu ndiyo akili kubwa ya mwisho ya mwanadamu. Tunasahau kuwa mabaya tunayokutana nayo yanafanya kazi kwa Manufaa ya hatma zetu. Unaweza fukuzwa kazi usijue kumbe ndio unaelekea katika kazi bora zaidi, unaweza kuachwa na mtu uliyempenda sana ukadhani ndiyo mwisho wa maisha kumbe Mungu amekuandalia mtu mwingine mwenye mapenzi ya dhati mtakayefikia malengo ya kujenga familia, unaweza kukataliwa na kutengwa na ndugu kumbe Mungu amekuandalia watu-baki watakaofanikisha ufikie malengo yako pasipo masimango ya ndugu, hata rafiki wanaweza kukusaliti kumbe Mungu amewaondoa makusudi ili kukuepusha na mabaya waliyoyapanga juu yako. Sasa usimlaumu Mungu ukadhani anakuzidishia matatizo, hapo anatafuta njia ya kuyaondoa hayo matatizo.
Mshukuru Mungu kwa Kila Jambo, kwakuwa hajawahi kukuwazia mabaya. Anakuwazia mema siku zote
Nimeipenda sana hadithi hii.
ReplyDeleteNimependa pia Maneno kuhusu mabaya hutokea ili kufanya Kazi kwa ajili ya hatma zetu nzuri
Ni kweli kaka kila jambo linatokea kwa sababu, Asante pia kwa kuisoma. Be blessed
DeleteNimefarijika na hii hadithi na nimejifunza jambo moja kubwa sana kwamba kila jambo linalotokea ni kwasababu maalamu Mungu amekuandalia
ReplyDelete