Ufugaji wa kuku wa asili ni nyenzo muhimu
katika kupambana na wimbi la umasikini kwa
kuongeza kipato cha kaya. Hata hivyo, pamoja na
soko la uhakika, bado ufugaji kuku haujaweza
kutumika ipasavyo kupambana na umaskini
unaowakabili Watanzania wengi. Ni mazoea kwa
jamii nyingi hapa Tanzania kufuga kuku wa asili
kama sehemu ya mila na desturi zao. Kuku wa
asili amekuwa akifugwa bila ya kupatiwa
huduma muhimu kama makaazi bora, chakula
cha ziada, tiba, kinga za magonjwa mbali mbali.
Muhtasari huu unatoa muongozo wa ufugaji wa
kuku wa asili ili uweze kuzalisha na hatimae
kukuza kuku kwa wingi.
Dondoo ya 1
Usafi wa vyombo na mazingira ya kuku
Uchafu ni mama wa magonjwa, hivyo zingatia
haya;
1. Vyombo vya chakula na maji visafishwe
mara kwa mara kwa maji safi na sabuni.
2. Pumba au chakula kilicholowana na
kuchanganyika na kinyesi cha kuku
kitolowe na kufukiwa.
3. Choma moto au zika kwenye shimo refu
kuku waliokufa kwa ugonjwa.
4. Usifuge kuku na ndege wa jamii nyingine
kwa mfano bata katika banda moja.
5. Ondoa mbolea mara kwa mara kutoka
katika banda la kuku.
6. Tumia dawa za kuulia vimelea kusafishia
banda na upake chokaa angalau mara
moja kwa mwaka.
7. Ziba matundu yote yanayoweza kuruhusu
panya na wanyama wakali kama vicheche
kuingia katika banda la kuku.
Dondoo ya 2
Magonjwa na kinga kwa kuku wote
Ndui ya kuku
Huathiri sana vifaranga wanaokua na ujitokeza
kwa wingi wakati wa mvua za muda mrefu.
Husababisha vivimbe katika uso/ kishungi na
hata sehemu nyengine zisizo na manyoya.
Mdondo/kideri
Mdondo, au kwa majina mengine lufuo, au kideri
ni ugonjwa hatari katika magonjwa ya kuku wa
asili. Ni ugojwa wa virusi ambao huathiri kuku
wa rika zote, huweza kuangamiza kuku wote
kijijni.
Ukosefu wa vitamini A
Ugonjwa huu husababisha macho kuvimba na
kutoa uchafu mziito kama sabuni iliyolowana.
Kuku wenye dalili hizi hawaponi na hata kufa.
Ugonjwa hujitokeza baada ya kipindi kirefu cha
kiangazi kwa ajili ya ukosefu wa majani mabichi.
Kosidiosisi
Huathiri kuku wa umri wowote lakini huuwa
zaidi vifaranga na kuku wanaokua. Kuku
hudhoofika, manyoya huvurugika na kuku huwa
kama wamevaa koti. Kuku huarisha damu au
kinyesi cha kahawia na huzubaa na kuonekana
kama wamevaa koti.
Viroboto, chawa na utitiri
Hawa ni wadudu wa nje wanaoshambulia ngozi.
Huweza kusababisha ugonjwa kutokana na
kunyonya damu. Viroboto hushambulia kichwa
na kunata huku wakinyonya damu. Viroboto
huuwa vifaranga. Chawa na utitiri hughasi kuku
hadi wakashindwa kutaga na kuatamia.
Minyoo
Minyoo huweza kudhofisha kuku na kuwafanya
waweze kuugua maradhi mengine kirahisi.
Muone mtaalaam ukihisi kuku wako wana
minyoo.
Dondoo ya 3
Chakula cha ziada
1. Wapatie vifaranga nyongeza ya protini kwa
kuwachanganyia vumbi la dagaa au
vichwa vya dagaa vilivyotwangwa kwenye
pumba za mahindi.
2. Changanya kikombe kimoja cha vumbi la
dagaa na vikombe vitano vya pumba za
mahindi (tumia kikombe kidogo cha chai).
3. Mchwa na wadudu wengine wanaweza
kutumika kama nyongeza ya protini.
4. Vuna mchwa kwenye vichuguu au
tengeneza mchwa katika njia za mchwa.
5. Kutengeneza mchwa: changanya kinyesi
cha ng’ombe na majani makavu, mabua
ya mahindi au maranda ya mbao katika
chungu au ndoo ya zamani.
6. Mwagia maji hadi kila kilichomo kilowane
kisha weka katika chombo kama ndoo au
chungu. Weka chombo chako katika njia
ya mchwa ukikigeuza juu chini na subiri
hadi kesho yake asubuhi, kisha beba vyote
vilivyomo na uwamwagie kuku mahali
walipo.
Dondoo ya 4
Utotoleshaji wa vifaranga
Chagua jogoo bora na tetea bora kuzalisha kuku.
Sifa za jogoo bora
1. Awe na umbo kubwa, awe ukiko mzuri na
usioangukia upande mmoja.
2. Apende kuwa na himaya yake. Ukimpata
jogoo mwenye sifa hizi mueke yeye na
matetea kumi. Hivyo ukiwa na matetea
ishirini jogoo wawili wanatosha.
Sifa za tetea bora
Tetea bora ni yule mwenye umbo kubwa,
mwenye uwezo wa kutaga mayai ya kutosha,
kuatamia na hatimaye kutotoa vifaranga.
Uhifadhi wa mayai
1. Weka mayai mahali safi na penye hewa ya
kutosha.
2. Tumia kasha lililokatwa na kujaza
mchanga mkavu na safi au kasha la
kuhifadhia mayai.
3. Weka sehemu butu ya yai iwe upande wa
juu na ile iliyochongoka itizame chini.
4. Andika namba au tarehe katika siku
lilipotagwa.
5. Mayai yakishatagwa yatolewe na
kuhifadhiwa na moja liachwe kwenye
kiota ili kumuita kuku kuja kutaga kesho
yake.
Kuatamiza mayai
1. Kuku awekewe mayai yatakayokuwa na
uwezo wa kuyaatamia na kuyatotoa yote.
2. Mayi 10 hadi 12 yanatosha kuatamia.
3. Mayai ya kuatamiza yasizidi wilki 2 toka
kutagwa.
4. Yai la mwisho kutagwa liwe la kwanza
kuchaguliwa hadi yapatikane mayai 10
mpaka 12, na apewe kuku wa kuyaatamia.
5. Mayai ya kuatamiza yasafishwe kwa
kitambaa kikavu na safi au kilichowekwa
spiriti
Kutotolesha vifaranga wengi kwa wakati
mmoja
1. Kama unataka kuku zaidi ya mmoja
watamie na kutotoa kwa mpigo fanya
yafuatayo;
2. Kuku wa kwanza akianza kuatamia
muwekee mayai yasiyo na mbegu mfano
mayai ya kuku wa kisasa au kuku asiye na
jogoo.
3. Rudia zoezi hilo hadi utakapofikisha kuku
watano kisha wawekee kuku wote mayai
yenye mbegu.
Dondoo ya 5
Matunzo ya vifaranga ili kuzuia vifo
Vifaranga wengi hufa kabla ya kufikisha miezi
miwili kutokana na magonjwa, baridi na kuliwa
na wanyama wengine. Ili kupunguza vifo vya
vifaranga wa siku 1 hadi miezi miwili zingatia
yafuatayo;
Ulinzi dhidi ya mwewe na wanyama wengine
1. Weka vifarang kwenye tega na kuwafunika
ili wasinde mbali wakati wa mchana.
Wape maji na chakula. Hakikisha
hawapigwi jua wala kunyeshewa mvua.
Wakati wa usiku walale na mama yao.
Chanjo ya mdondo kideri/lufuo
Kama tetea alichanjwa kabla ya kuanza kutaga
vifaranga wanaoanguliwa huwa na kinga ya
mdondo ya kuwatosha kwa wiki 3 za kwanza za
maisha yao. Wachanje vifaranga hao dhidi ya
mdondo wafikishapo umri wa siku 18.
Vifaranga ambao historia ya chanjo ya mama
haijulikani, wapewe chanjo ya mdondo siku tatu
baada ya kuanguliwa, rudia hadi wakifikisha
wiki tatu kisha uchanje kila baada ya miezi 3
Kinga dhidi ya kosidiosisi
Kinga ya kosidiosisi kwa vifaranga, itolewe hata
kama ugonjwa haujajitokeza.
1. Wape dawa ya amprolium kwa muda wa
siku tatu mfululizo mara wafikishapo siku
saba tokea waanguliwe kama kinga ya
kosidiosisi.
2. Dawa inaweza kutolewa hata kama
wamevuka umri huo. Fuata maelekezo ya
mtaalam juu ya kiasi cha dawa
kinachopaswa kuchanganwa katika maji
au pumba
3. Kama vifaranga wadogo wataonesha dalili
za kuzubaa kama kuvaa koti wapewe
dawa ya amprolium kwenye maji kwa
utaratibu ufuatao;
Dawa siku tatu mfululizo: usiwape kwa siku
mbili; gawa tena kwa siku tatu
Hitimisho
1. Hakikisha banda na vyombo vya chakula
cha kuku ni visafi kuepusha magonjwa.
2. Usichanganye kuku na bata katika banda
moja
3. Lisha chakula cha ziada hasa kwa
vifaranga.
4. Kideri, kosidiosisi, ndui na upungufu wa
vitamini A ni vyanzo vikuu vya vifo vya
kuku wako. Kumbuka kukinga kuku wako
dhidi ya magojwa haya.
5. Kumbuka kuchagua mayai ya kuatamiza
kama ilivyoelekezwa ili kuepuka kupata
mayai viza.
6. Vifaranga wadogo hadi wiki nane huhitaji
matunzo mazuri, fuata maelezo kuzuia
vifo.
7. Kumbuka ukiuza kuku wengi kwa mpigo
utaongeza mapato yako, jitahidi kuzalisha
vifaranga kwa wingi ili upate kuku wengi
baadae.
8. Muone mtaalam wa mifugo ulie karibu nae
kwa ushauri zaidi.
9. Soma maelezo haya mara kwa mara na
ufanye yalioelekezwa.
10. Washirikishe wengine katika kaya
yako ili nao wajifunze na kufanya hivyo
kukuza ufugaji na kipato cha familia.
0 comments:
Post a Comment